Header Ads

Stars imeshindwa kuvunja rekodi ya miaka 20 dhidi ya Zambia Cosafa Cup


Julai 5, 1997 kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid Karume,mechi ya Cosafa Cup Tanzania ilicheza dhidi ya Zambia ‘Chipolopolo’ na mechi kumalizika kwa matokeo ya sare ya kufungana 2-2.
Dakika ya 56 Edbily Lunyamila aliiandikia Stars bao lakini dakika ya 71 Masauko Tembo akaisawazishia Zambia, dakika ya 75 Hussein Masha akaifungia Stars bao kwa mkwaju wa penati na kuifanya Tanzania kuwa mbele kwa mabao 2-1. Dakika ya 83 Alex Zaba akaisawazishia Zambia na mchezo kumalizika kwa sare ya 2-2.
Miaka 20 baadae (Julai 5, 2017) kwenye mashindano hayohayo ya Cosafa Tanzania imekutana tena uso kwa macho na Zambia kwenye hatua ya nusu fainali ya mashindano ya mwaka huu.
Stars imeshindwa kusonga mbele kwenye mashindano ya Cosafa baada ya kupoteza mchezo kwa kufungwa 4-2 na kuiacha Zambia ikisonga mbele kucheza fainali ya michuano hiyo nchini Afrika Kusini.
Magoli ya Stars yamefungwa na Erasto Nyoni dakika ya 14 ambaye alifunga goli la kwanza kisha Simon Msuva akafunga goli la pili dakika ya 85 wakati magoli ya Zambia yakifungwa na Mwila dakika ya 44 kisha Shonga akafunga dakika ya 45+2 Zambia wakapata goli la tatu kwa mkwaju wa penati uliofungwa na Chirwa dakika ya 56 halafu Shonga akafunga bao la nne likiwa ni goli lake la pili dakika ya 68.
Mwaka 1997, michuano hiyo ilikuwa inapigwa kwa makundi baada ya kuchezwa mechi za mtoano na kulikuwa na mfumo wa nyumbani na ugenini.  Katika mashindano ya mwaka huo (1997) Tanzania ilimaliza katika nafasi ya nne huku Zambia wakiwa ndio mabingwa.
Tanzania ilimaliza ikiwa na pointi tatu baada ya kutoka sare katika mechi zake zote katika kundi lao, baada ya Zambia kuitoa Tanzania kwenye Cosafa 2017, Je itatwaa ubingwa kama ilivyofanya mwaka 1997?
Endapo Stars ingepata ushindi kwenye mchezo wa leo, ingevunja rekodi ya mwaka 1997 ambapo iliambulia sare ikiwa ni mashindano yaleyale ya Cosafa.

No comments