Header Ads

Sio Abdi Banda pekee, hawa hapa mabeki wasio na sifa ya ‘kubutuabutua’ barani Ulaya


Wanasoka wengi wamezoea kuwaona mabeki wa kati wakiosha ‘kubutua’ hasa linapokuja suala la timu zao kushambuliwa. Jambo hili limekuwa la kawaida sana kwa mashabiki na mara zingine kelele za kushangilia husikika pindi tukio kama hili linapotokea. Tumezoea kuwaona mabeki ambao huwa hawapendi masikhara langoni kwa kuuchezea mpira mfano Pepe, Zouma au Varane kwa nyakati zingine. Ila wapo mabeki ambao wamejaaliwa uwezo wa kuuchezea mpira sehemu yoyote bila woga.
Hapa Tanzania nimebahatika kuwatazama mabeki wengi ila Abdi Banda ni kijana ambaye anaonekana kujitahidi kuwa na uwezo mkubwa wa kuuchezea mpira sehemu yoyote hasa katika idara ya ulinzi ya timu yake hadi kufikia hatua ya kuwaogopesha mashabiki wa Simba na Taifa Stars. Banda mara nyingi ameonekana akiwapiga vyenga washambuliaji katika ‘Sita’ ya timu yake tena kwa ujasiri wa hali ya juu na amekuwa akifanikiwa licha ya makosa ya hapa na pale ambayo yamekuwa yakionekana.
Kipaji cha kuuchezea mpira kinakubalika zaidi kwa timu ambazo hucheza mpira wa kufunguka mfano Barcelona, Monaco, Arsenal, Spurs na Bayern Munich. Kisa kikubwa cha Pique kurejea Barca kutoka Man United ni uwezo wake mkubwa wa kuuchezea mpira na sio kubutua butua hovyo. Kutokana na hili leo hii nimejaribu kuwatizama mabeki wa kati ambao wameonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kuuchezea mpira katika zile ligi 5 bora barani Ulaya msimu uliopita.
SERIE A anasimama Leonardo Bonucci wa Juventus ambaye ni beki wa kati mwenye uwezo mkubwa wa kuuchezea mpira akiwa katika eneo la hatari la timu yake.  Bonucci alitajwa kwenye kikosi cha mwaka 2016 cha UEFA kutokana na uwezo wake mkubwa wa kupiga pasi zenye madhara kwa timu pinzani. Msimu uliopita kwenye Serie A alipiga pasi zilizofika sehemu iliyokusudiwa kwa 87% na hii ni kutokana na kujiamini kwake hasa akiwa na mpira mguuni. Bonucci ni beki aliyewaniwa na Chelsea na Barca bila mafanikio.
BUNDESLIGA yupo Mats Hummels anayecheza FC Bayern Munich ambaye anatajwa na vyombo vingi vya habari kama beki bora wa kati mwenye uwezo mkubwa wa kuuchezea mpira eneo lolote hata kwenye mstari wa goli lake. Uwezo wake ulimfanya Bayern wamchukue kutoka Dotmund. Beki huyu alilelewa kwenye Academy ya Bayern Munich na kucheza Dotmund kwa mkopo kabla ya kusajiliwa na timu hii moja kwa moja 2009. Katika michezo 27, Hummels amepiga pasi 2047 huku 1677 akizipiga kwenda eneo la mbele.
EPL hatuna shaka na Jan Vertonghen wa Tottenham Hotspur. Huyu ni Beki bora wa kati anaejua kuuchezea mpira na kujiamini kuliko beki yoyote pale EPL hasa kwa kiwango alichokionesha msimu uliopita. Kubutua mipira ni jambo gumu kwa mbelgiji huyu ambaye anafanya kazi na Mauricio Pochetino. Mabeki ambao wanafukuzana na Jan ni John Stones wa Man City na Laurent Konscenly wa Arsenal. Jan Vertonghen ni mgumu sana kupoteza pasi kwani ‘clear’ pasi aliyopiga kwa 75% zinadhihirisha hili.
LA LIGA yupo pia Sergio Ramos wa Real Madrid. Naweza kusema huyu  ndiye beki wa kati anaeyejiamini kwa sasa barani Ulaya. Ramos alianzia kucheza upande wa kulia kabla ya kuhamia katikati na hii ilikuwa baada ya kuhamia Madrid. Tulizoea sana wachezaji kutoka Lamasia wakisifika kwa uwezo wao mkubwa wa kuuchezea mpira eneo la ulinzi ila Ramos misimu ya karibuni amekuwa bora sana kuliko hata Gerald Pique na Mascherano ambao wamekuwa wakimwagiwa sifa.
LEAGUE 1, Marquinhos ni beki mzuri sana wa Kibrazil anayekipiga pale PSG. Japokuwa amekuwa na uwezo mkubwa wa kucheza nafasi ya kulia ila hata nafasi ya beki wa kati imemfanya aingie kwenye orodha hii ya mabeki wa kati ambao wamejaaliwa kipaji cha kuuchezea mpira na sio kubutua butua bila mpangilio. Marquinhos ana uwezo mkubwa wa kupiga chenga na kukaba pia bila kucheza faulo. Marquinhos ndiyo beki aliyecheza mechi nyingi pale PSG akiwa mbele ya Thiago Silva kwa mechi 2.

No comments