Header Ads

Rooney arejea nyumbani na pesa pamoja na heshima


Kocha Jose Mourinho amekiri hakuweza kumzuia Rooney alipotaka kurudi Everton, Mourinho amekiri kuwa hata yeye ni mshabiki mkubwa wa Wazza lakini kumzuia kurudi Everton lilikuwa jambo gumu kwake, naamini kama Mourinho ameshindwa hakuna ambaye angeweza.
Tayari mshambuliaji huyo ameondoka Manchester United na kurudi tena katika klabu yake ya zamani ya Everton kwa mkataba wa miaka miwili jambo ambalo halijamshangaza mtu kwani Rooney amerudi sehemu moyo wake ulipo baada ya kupata pesa kazini alikotoka.
Ni wazi kwamba Rooney amerudi Everton kwa wakati sahihi na kitu sahihi, Rooney ni mshabiki wa Everton haswa na klabu hiyo iko moyoni mwake na Manchester alienda kwa ajili ya kazi ya soka aliyoifanya kikamilifu na baada ya umri kwenda amerejea nyumbani na heshima kubwa.
Miaka 13 iliyopita Wazza alijiunga na Manchester United, kocha wa United kipindi hicho babu Sir Alex Ferguson alisema “tumepata kinda bora kuwahi kumuona katika miaka 30 iliyopita” dunia iliamini maneno ya babu Fergie baada ya Rooney kuanza kukanyaga nyasi za Old Trafford.
Magoli 253 kati ya michezo 559 nani anaweza kubisha kwamba huyu ndio mwanasoka bora wa United kuwahi kutokea miaka 10 iliyopita?! Rooney akiwa na United amebeba karibia kila kombe la vilabu unalolijua duniani.
Kichwa cha Rooney kametikisa nyavu mara 30, mguu wa kulia mara 195 wa kushoto mara 28, rekodi zake zinaonesha tu alichokwenda kufanya Manchester United hakika aliutoa mwili wake wote kufanya kazi iliyompeleka hapo huku akijua atatakiwa kurudi nyumbani siku moja.
Makombe matano ya Epl, amechukua Europa, amechukua Champions League amechukua kombe la FA, na pesa nyingi amechukua akiwa na United, baada ya kupata vitu vyote hivyo unabaki kufanya nini na umri wako ni miaka 31 kama sio kurudi nyumbani kusaidia ndugu na jamaa zako?
Ukimsikiliza Rooney akiongea baada ya kurudi Everton utaelewa ni jinsi gani amefurahia uhamisho huo “najisikia faraja sana kurudi hapa na nina hamu kubwa kukutana na wenzangu katika klabu hii niliyokulia na kuipenda” alisema Rooney.
Goodison Park sio mahala pageni kwa Wazza kwani alishacheza michezo 77 katika dimba hilo la Everton na kurudi kimiani mara 17 kabla ya uhamisho wake wa £27 kwenda katika kazi ya kuitumikia Manchester United mwaka 2004.
Sisi vijana tuliozaliwa miaka ya 90 na kuendeleza hatukuona sana ubora Bobby Charton wala Kenny Danglish, Rooney ndio mwanasoka bora wa Uingereza kuwahi kumshuhudia akicheza soka na hakika mashabiki wa United watammiss Wazza huku jina lake likiwa kwenye vitabu vya rekodi za klabu hiyo.

No comments