Header Ads

KUSAJILI WACHEZAJI 16 KWA MKUPUO, SINGIDA UNITED LAZIMA WAKUBALIANE NA HALI HALISI


KIKOSI cha Singida United kimesajili jumla ya wachezaji 16 wapya kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

Singida United ndiyo imepanda daraja msimu huu ikitokea Ligi Daraja la Kwanza na bahati nzuri moja kwa moja wamepata wadhamini kadhaa.

Kampuni ya Kubashiri ya SportPesa imekuwa ya kwanza kujitokeza kuidhamini Singida United kwa kutoa kitita cha Sh milioni 250 kwa mwaka huku wengine kama Puma nao wakiingia kutoa sapoti ya udhamini.

Wakati Singida United ikiwa imeanza maandalizi kwa ajili ya msimu mpya, tayari imeshaanza kuwa gumzo kutokana na kusajili wachezaji wengi wapya lakini pia ule uamuzi wa kumchukua Kocha Hans van Der Pluijm.

Kama utataja kocha bora ndani ya misimu minne katika Ligi Kuu Bara, Pluijm raia wa Uholanzi ndiye kocha bora kabisa zaidi ya wengine kwa kuwa amebeba ubingwa na Yanga zaidi ya mara moja katika muda huo na kikosi chake kilionyesha uwezo mkubwa.

Usajili wa wachezaji 16, unathibitisha ile kauli yangu ya awali, kwamba Simba waliosajili wachezaji 12 wapya, hawakukosea kwa kuwa unahesabu wangapi waliotoka lakini pia unaangalia mbele ni michuano gani inafuata.



Simba waliangalia Ligi Kuu Bara, waliangalia Kombe la Shirikisho pia michuano ya kimataifa. Ndivyo ilivyo kwa Singida United ambao wanaangalia Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho lakini wakifikiria kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa.

Kwa hali ilivyo sasa, baada ya kukamilika kwa usajili wa wachezaji 25, Singida United imetangaza kufunga usajili lakini presha kubwa sasa inaangukia kwa Kocha Pluijm.

Kama nilivyoeleza kwanza, hakuna anayeweza kukataa kwamba Pluijm ni kocha bora lakini presha kwake inaweza kuwa kubwa saizi ya kati au kubwa sana kulingana na mazingira.

Kwa sasa anafanya kazi ya kuunganisha kikosi chake chenye wachezaji 16 wapya kati ya hao saba wakiwa kutoka nje ya Tanzania na tisa pekee ndiyo wale waliopanda na timu.

Utaona wachezaji 16 wanakwenda kuzoea mazingira mapya wakiwa saba na tisa wamekutana hapo na tisa wengine ambao wamewakuta.

Muunganiko huu wa makundi matatu haiwezi kuwa kazi rahisi kwa Pluijm ingawa kuna mambo mawili lazima utayaona katika kikosi hicho.

No comments