Umoja Wa Vilabu Vya Waandishi Wa Habari Tanzania ( MCT, UTPC na THRDC) Walaani Vikali Serikali Kulifungia Gazeti La Mawio
TAMKO LA PAMOJA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU KUFUNGIWA KWA GAZETI LA MAWIO NA HALI YA UHURU WA HABARI NCHINI
UTANGULIZI
Baraza
la Habari Tanzania (MCT), Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu
Tanzania (THRDC) na Umoja wa Vilabu vya Habari Tanzania (UTPC) kwa
pamoja tunalaani vikali kufungiwa kwa Gazeti la Mawio na Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe Juni 15,
2017. Gazeti limepigwa marufuku kuchapishwa na kuwekwa katika mzunguko
kwa miaka miwili.
MAKOSA WANAYOTUHUMIWA KUFANYA
Gazeti
la Mawio limefungiwa siku ya tarehe 15 Juni 2017, baada ya kutoa toleo
lake lenye namba 196 la tarehe 15-21Juni, 2017.Waziri ametumia sheria
mpya ya Huduma ya Vyombo vya Habari, 2016 kulifungia gazeti la Mawio kwa
madai ya kukiukwa vifungu vya sheria hiyo na “Agizo la Mhe Rais” kuhusu
kutowahusisha Marais wastaafu na sakata la uporaji wa rasilimali madini
nchini. Gazeti hili limeshutumiwa kutenda makosa mawili; kosa la kwanza
chini ya kifungu cha 50 na 59 cha Sheria ya Huduma za Habari Namba 2
ya 2016 na kosa la pili kukiuka “ Agizo la Rais laTarehe 14/6/2017.. “
kama ifuatavyo;
(ii) Kuchapisha Picha za Marais Wastaafu
Waziri
alidai kuwa, gazeti hilo limechapisha picha na majina ya marais
waliopita kwa kuwahusisha na kashfa ya rushwa katika mikataba ya madini
kati ya Serikali na wawekezaji.
Waziri anasema kuwa hawakufurahishwa na picha za marais wastaafu ambazo ziliwekwa kwenye ukurasa wa mbele.
(i) Kuchapisha Makala Kuhusu Uporaji wa Madini kinyume na Agizo la Rais
Kosa
la pili ni kuchapisha makala ambayo ilichapishwa katika ukurasa wa 12
wa gazeti hilo kinyume na “Agizo la Rais la tarehe 14/6/2017.
Linalowataka watanzania kuacha kuwataja au kuwahusisha marais wastaafu
na sakata la upoteaji wa rasilimali madini”.
Makala
hiyo ni andiko lililosheheni historia ya jinsi viongozi mbalimbali
walivyoshiriki katika usimamizi wa uwekezaji katika sekta ya raslimali
madini.
UCHAMBUZI KUHUSU TUHUMA HIZI NA HATUA YA KULIFUNGIA GAZETI
Itambulike
kuwa hii si mara ya kwanza kwa magazeti na vyombo vya habari kufungiwa
na Waziri katika nchi yetu kwa kutumia sheria mbalimbali kandamizi
hasa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 iliyofutwa mwaka 2016 na kuridhiwa
na Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya 2016. Magazeti kadhaa
yalifungiwa katika siku za nyuma ikiwemo Mwananchi, Mawio, Mwanahalisi
na Mtanzania.
Kwa
upande wa Gazeti la Mawio hii ni mara ya pili kusimamishwa. Januari 15,
2016 gazeti hili lilipigwa marufuku kabisa kupitia Tangazo la Serikali
(GN) Namba 55 la 2016. Hata hivyo gazeti hilo liliishtaki Serikali kwa
mafanikio katika kesi namba. 15 ya 2016 na hatimaye likaweza kuendelea
na machapisho yake.
Itambulike
kuwa kwa muda mrefu tumekuwa tukipinga utaratibu wa kisheria wa kumpa
Waziri mamlaka makubwa katika sekta ya habari.
Sheria
iliyopita na ya sasa havina tofauti yoyote hasa katika mamlaka ya
Waziri kulifungia gazeti pekee na kwa makosa atakayoyaona yeye ni
kinyume na maslahi ya umma. Sheria hii mpya imeendelea kumfanya Waziri
awe Mhariri Mkuu, Mlalamikaji, Mpelelezi, Mwendesha Mashtaka na Hakimu
kwa wakati mmoja.
Kifungu
cha 59 cha sheria ya huduma za habari imetumika kulifungia Mawio kwa
madai kuwa kuchapisha picha za viongozi wastaafu ni kinyume na maslahi
ya umma.
Kwa
mujibu wa Ibara ya 18 ya Katiba ya Tanzania Watanzania wana uhuru wa
kutoa maoni na kupashana habari kuhusiana na mambo mbalimbali yanayohusu
maisha yao.
Kitendo
cha kuzuia watanzania au vyombo vya habari visichapishe picha za
viongozi wastaafu hasa katika mijadala ya kitaifa ambayo inahusu mambo
yaliyotekea wakiwa madarakani ni kuwaziba watanzania midomo katika
sakata la vita dhidi ya wizi wa madini Tanzania.
Katika
kosa la pili gazeti hilo lilitumia makala ya Mbunge mmoja na mtaalamu
wa sheria za madini nchini yenye maelezo juu ya mambo muhimu katika
kumsaidia Mhe. Rais katika vita ya uporaji wa rasilimali madini.
Vyombo
vya habari kama watu wengine wana haki ya kutoa habari kama wanadhani
ina maslahi kwa umma ilimradi hazikiuki sheria. Tumeshangazwa kuona
Waziri kitaaluma ni Mwanasheria ametumia Agizo la Rais Kama sheria
kitendo ambacho ni hatari kwa mustakabali wa Taifa kama kila
kitakachoagizwa na kiongozi mkuu kitachukuliwa kama ni sheria.
Hata
hivyo kwa mujibu wa Mawio, Agizo la Rais kuhusu kuzuia marais wastaafu
wasitajwe au kujadiliwa kwenye sakala la madini lilitoka wakati tayari
gazeti hilo toleo la tarehe 15/6/2017 lilishakuwa limeshachapishwa na
kusambazwa kwa mawakala nchi nzima tarehe 14/6/2017 wakati ambapo ndipo
Agizo la Rais lilitoka tarehe hiyo hiyo 14.
Taarifa
rasmi ya Mkurugenzi wa Idara ya habari-MAELEZO na msemaji mkuu wa
Serikali ilinukuu Kifungu cha sheria cha 50 (a) (b) (c) (d) na (e) kuwa
ndicho kifungu kilichokiukwa na gazeti la Mawio kwa mujibu wa taarifa ya
Waziri Dr. Harrison Mwakyembe. Aidha, kifungu kilichotumiwa na waziri
kutoa adhabu hakiendani na kifungu kilichotamka kosa lililotendwa na
gazeti la Mawio.
Kwa
mujibu wa kifungu kilichotumika, mamlaka yenye uwezo wa kutoa adhabu ni
mahakama baada ya kumsikiliza mtuhumiwa jambo ambalo katika maamuzi ya
Waziri Mwakyembe halikufanyika ukiachilia mbali kwamba yeye sio
mahakama.
Ikumbukwe
kwamba, mamlaka pekee yenye uwezo wa kutoa haki katika Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ni Mahakama kwa mujibu wa Ibara ya 107 (A) (1) ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hivyo waziri kutoa adhabu kama hii amekiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Kifungu
alichotumia kutoa adhabu hakielezi kosa lililotendwa na gazeti la Mawio
na kisheria adhabu haiwezi kutolewa bila kuwepo kosa (no punishment
without law kwa kilatini Nullum Criminem Sine Lege). Waziri ametoa
adhabu kwa gazeti la Mawio bila kufuata misingi ya sheria ili hali yeye
mwenyewe ni mwanasheria.
Ikumbukwe
mpaka sasa kwambakuzuia kujadili watu au juu ya masuala ambayo
hayakuwekwa katika ripoti mbili za kamati ya Mhe Rais juu ya kashfa ya
madini, haiondoi haki na wajibu kwa watanzania kama ilivyoanishwa
katika katiba ya nchi kama ifuatavyo;
•
Kila mtu anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake Ibara ya
18(a). Makala iliyochapishwa katika ukurasa wa 12 ni maoni ya mwandishi
wa makala hiyo kwa mujibu wa kifungu hiki.
•
Kila mtu amepewa haki wakiwemo waandishi wa habari kutafuta, kupokea na
kutoa taarifa kama inavyoelezwa katika Ibara ya 18 (d) ya Katiba.
Wanahabari ni sehemu muhimu katika maendeleo ya taifa letu na wamekuwa
kiungo kizuri cha utekelezaji haki hii.
•
Kila Raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wowote kuhusu matukio
mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na shughuli muhimu
kwa wananchi Ibara ya 18 (b). Suala la Madini ni tukio muhimu kwa
maisha ya Mtanzania na gazeti la mawio lilikuwa katika kufikisha taarifa
mbalimbali zinazohusiana na sakata hili la madini.
•
Katiba ibara ya 27 (1) imempa wajibu kila Mtanzania wajibu wa kulinda
rasilimali asili za nchi. Hivyo pamoja na kuwa kuna ripoti mbili za
kamati, bado watanzania wengine wana wajibu wa kumsaidia Mhe. Rais
katika kulinda rasilimali za nchi kama gazeti la Mawio lilivyofanya kwa
kuruhusu watanzania watoe taarifa wanazoona ni muhimu kumsaidia Rais
katika sakata hili.
Tumebaini
pia hakukuwa na utaratibu mzuri wa kuwasikiliza viongozi wa Mawio
kwani Idara ya Habari iliwasiliana kwa njia isiyo rasmi na Mhariri wa
Mawio bila ya kutoa barua yoyote ya kiofisi. Pamoja na kwamba hakukuwa
na mawasiliano yoyote ya kiofisi zaidi ya simu, Mawio waliandika barua
ya kuelezea sababu za kuchapisha gazeti lao na taarifa husika.
Moja
ya sababu ni kuwa gazeti lilipishana na Agizo la Rais. Maanake Agizo
liliwafikia wakati tayari gazeti limekwishachapwa na kusambazwa kwa
mawakala.
Nguvu kubwa kama hizo alipewa Waziri pia katika Sheria ya Magazeti ya 1976 na sasa imeletwa katika Sheria ya Huduma za Habari.
Waziri chini ya sheria hii mpya anafanya kazi kama mhariri mkuu, mlalamikaji, mchunguzi, mpeleka mashtaka na jaji.
Kwa
mfano, Kifungu cha 59 cha Sheria ya Huduma za Habari inasema kwamba,
"Waziri atakuwa na uwezo wa kuzuia au kuweka vikwazo kwa uchapishaji wa
maudhui yoyote ambayo yanahatarisha usalama wa taifa au usalama wa
umma."
Hiki
ni kipengele pekee ambacho Waziri anaweza kutumia kupiga marufuku
gazeti. Kifungu hicho kinampa nguvu kubwa mno mtu moja kuamua makosa
yanayofanywa chini ya Sheria ya Huduma za Habari na kuwa muamuzi wa
makosa hayo pia. Ni kinyume na misingi ya sheria za utawala bora.
Licha
ya ukweli kwamba sheria hii ni mbaya sana na ni hatari kwa uhuru wa
kujieleza na vyombo vya habari kwa ujumla, tunaona hakuna uwezekano
wowote kwamba machapisho hayo yameweza kuuweka "usalama wa taifa au
usalama wa umma hatarini”.
Badala
yake, uchapishaji wa picha za viongozi wastaafu wa nchi na makala
iliyoundwa vizuri ikionyesha namna ambavyo sheria mbaya katika sekta ya
madini zilipitishwa katika nchi yetu kipindi cha uongozi wao inaweza
kutumika vyema na serikali, Bunge na wadau wengine ili kupata ufumbuzi
sahihi katika usimamizi wa rasilimali zetu.
Kufungiwa
kwa Mawio si tu kumekiuka sheria zetu kuhusu uhuru wa kujieleza lakini
pia kimataifa imevunja Ibara ya 19 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za
Kiraia na Kisiasa (ICCPR) na Mkataba wa Afrika ambao Tanzania imeridhia.
Kwa
uzuiaji huu idadi kubwa ya Watanzania wamenyimwa haki ya kupata taarifa
na hivyo inapunguza kiwango cha uwazi kwa viongozi wa serikali kwa
sababu waandishi wa habari na vyombo vya habari kwa ujumla ni
waangalizi wa utendaji wa serikali.
Kwa
ujumla hatukuona sababu kubwa ya kulifungia gazeti hilo kwani tuhuma
zote zilikuwa zinazungumzika lakini katika njia ambayo ingehusisha
makundi kadhaa katika sector ya habari badala ya kumwachia Waziri awe
mlalamikaji, mwendesha mashtaka na mwamuzi kwa wakati mmoja.
WITO NA USHAURI WETU
•
Serikali itengue uamuzi wake wa kulifungia gazeti la Mawio kwani
umeenda kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na
Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016 ambayo kimsingi haimpi mamlaka
waziri kutoa adhabu aliyoitoa.
•
Juhudi za serikali katika kuhakikisha uchumi unakua na juhudi za
kupambana na rushwa lazima ziende sambamba na viongozi kuwa wavumilivu
na kukubali kukosolewa kwa mambo ambayo ni muhimu katika kufikia
malengo na matarajio hayo.
•
Ili kutimiza nia ya Rais wetu ya dhati katika kukabiliana na
watuhumiwa wote wa kashfa za madini, yampasa kuruhusu wananchi
kuwajadili kwa uhuru wale wote wanaotuhumiwa kuhusika bila kujali kwamba
wametajwa katika taarifa ya Kamati au la.
•
Tunamshauri Rais atambue kuwa hiki kizuri anachokifanya leo katika
kulinda rasilimali asili, kinaweza kuwafanya wananchi kwa nia nzuri
kabisa kuhoji viongozi wa zamani walifanya nini kwa kuwa walikuwa na
jukumu kubwa katika kushawishi aina ya usimamizi wa rasilimali wakati wa
uongozi wao.
•
Ikumbukwe kwamba vyombo vya habari, ikiwa ni pamoja na Magazeti hufanya
shughuli zao kwa mujibu wa sheria za Tanzania, hasa Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Katiba inasema wazi chini ya
Ibara ya 18 kwamba Watanzania wote wana haki ya kutafuta, kupokea na
kutoa habari na maoni kwa njia yoyote.
•
Kwamba serikali inapaswa kuondoa marufuku yake dhidi ya Mawio
kuzingatia kwamba sheria hii inakiuka misingi ya kidemokrasia na
inajenga picha hasi ya nchi yetu kwa jumuiya ya kimataifa.
•
Ni wakati muafaka sasa kwa Sheria ya Huduma za Habari, 2016 kufanyiwa
marekebisho ili kuhakikisha kwamba vifungu vyake vinaendana na matakwa
ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inatoa ukakika wa
uhuru wa kujieleza.
•
Tunamshauri Mhe Rais avione vyombo hivi vya habari kama wabia wazuri
katika kupambana na rushwa nchini , na asikubali kuona wasaidizi wake
wanachukua hatua za kuwajengea hofu waandishi wa habari katika
kuhabarisha mambo yanayohusu ufisadi na uhujumu uchumi.
•
Vyombo vyote vya habari na wanahabari waweke tofouti zao pembeni na
waamke kupigania uhuru wao wa kufanya kazi zaao kama katiba ya nchi
inavyotaka.
•
Kwamba waandishi wa habari na wahariri wachukue kwa uzito masuala yenye
maslahi ya Taifa na pia kusimamia maadili ya taaluma zao.
•
Tunashauri Sheria ya Huduma za Habari ifanyiwe marekebisho ili kuondoa
vifungu vinavyompa mtu mmoja mamlaka ya kufungia chombo cha habari na
kuweka mfumo shirikishi utakaoshirika wadau wengine wa vyombo vya habari
katika kufuatilia makosa yanayofanywa na vyombo vya habari
•
Kutokana na kuwa hakuna sehemu yoyote ya kupeleka rufaa dhidi ya
maamuzi ya Waziri katika sheria ya huduma za habari ya 2016, endapo
hakutakuwa na mazungumzo na waziri, tutakwenda mahakamani kwa
kushirikiana na Mawio kuonyesha haki zilizokiukwa katika kulifungia
gazeti hili.
Imetolewa kwa pamoja kati ya MCT, UTPC na THRDC leo Juni 18, 2017
...............................................................
Pili Mtambalike
Kaimu Katibu Mtendaji Baraza la Habari Tanzania (MCT)
Onesmo Olengurumwa
Mratibu wa Taifa, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC)
Deogratius Nsokolo,
Rais – Umoja wa Vilabu vya Waandishi Habari Tanzania-UTPC
Post a Comment