Kutoka kwa Zitto Kabwe kuhusu stori za kugombea Urais wa TFF
Mbunge wa Kigoma Mjini na kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe leo June 19 2017 ameamua kuweka wazi msimamo wake kuhusu stori zilizoenea kuwa atachukua fomu ya kugombea Urais wa shirikisho la soka Tanzania.
Wengi walikuwa wanataraji kusikia au kuona muda wowote kutokea sasa, baada ya kamati ya uchaguzi ya TFF kutangaza muda wa kuchukua fomu, Zitto Kabwe angechukua fomu ya kugombea nafasi hiyo, leo June 19 2017 ametangaza msimamo wake kuhusiana na hilo.
“Ijumaa ya Aprili 21, mwaka huu, gazeti la michezo na burudani nchini, Mwanaspoti, liliandika habari kwenye ukurasa wake wa kwanza yenye kichwa: “Zitto ajitosa Urais TFF, Rage amkubali.”
“Upande wangu, licha ya kwamba habari hiyo ilichapishwa bila kupata maoni yangu, lakini haikuwa ngeni. Hii ni kwa sababu kabla ya habari hiyo nilikuwa nimeshapokea maombi kutoka kwa watu mbalimbali, wakiwemo viongozi wakubwa wakinitaka nigombee Urais TFF”
“Baada ya habari hiyo kuchapishwa na kupata umaarufu mkubwa, nilipokea maombi mengi zaidi pamoja na shinikizo lenye kunitaka muda ukifika wa uchukuaji fomu, nijitokeze nichukue fomu ya kuwania Urais TFF”
“Msukumo ni mkubwa na maswali ni mengi kipindi hiki ambacho dirisha la uchukuaji fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi TFF limefunguliwa”
“Kila ombi na shinikizo ambalo nimepokea, nimelibeba kwa unyenyekevu mkubwa. Bila shaka wanaoniomba na kunishinikiza wanavutwa na mambo mawili; mosi, soka letu kutoleta nuru kwa Watanzania. Pili, imani kubwa kwamba kupitia uongozi wangu nuru ya soka letu itadhihirika”
“Hata hivyo, yapo mambo mawili nimeyatafakari; Mosi, mahitaji ya soka letu na nguvu ya maarifa inayohitajika kulikwamua. Pili, nafasi yangu kama mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini na Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo”
“Kuhakikisha kazi ya kulikwamua soka letu inafanikiwa na nuru inadhihirika kwa wapenda soka wote nchini, inahitaji uwekezaji mkubwa wa muda, vilevile uwekezaji mkubwa wa maarifa ya kiuongozi”
“Soka la Tanzania lipo hapa kwa sababu ya uwekezaji usioridhisha wa maarifa ya uongozi, hiyo inatokana pia na viongozi wanaopata nafasi ya kulitumikia shirikisho letu la mpira wa miguu nchini, kutowekeza muda wao barabara kwenye soka”
“Nikiwa Kiongozi wa ACT-Wazalendo, ninadaiwa mambo mawili, uwekezaji wa muda na uwekezaji wa maarifa ya kiuongozi ili kukiandaa vema chama chetu kushiriki uchaguzi kati ya miezi 28 mpaka 40 inayokuja”
“Mwaka 2019, Chama kitashiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa, mwaka 2020, Chama chetu kitashiriki Uchaguzi Mkuu”
“Hivyo basi, kwa kuongezea na uwakilishi wangu wa Jimbo la Kigoma Mjini ambako Chama chetu kinaongoza Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, naona kuwa lipo eneo ambalo nitashindwa kulitimizia wajibu wake nikivaa kofia ya tatu ya Urais wa TFF”
“Nimetafakari na kuchukua uamuzi kwamba Uongozi wa ACT-Wazalendo na Ubunge ni nafasi ambazo ninazo tayari, wakati Urais TFF ni nafasi mpya”
“Kwa hali hiyo na kwa mapenzi makubwa ya soka la Tanzania, nimeamua nisichukue fomu ya kugombea Urais wa TFF, kwani naweza kuomba kazi ambayo nitashindwa kuitumikia kwa muda wa kutosha kutokana na majukumu yangu kwenye Chama na ubunge”
“Uamuzi huu umezingatia mapenzi makubwa kwa soka letu. Nikijitokeza kuwania Urais wa TFF leo halafu nikakosa muda mzuri wa kutimiza matarajio ya wapenda soka nchini, utakuwa usaliti mkubwa kwa maendeleo ya soka la Tanzania”
“Nawashukuru wote walioniomba na kunishinikiza nichukue fomu. Nawaambia kuwa kwa sasa tujielekeze kupata viongozi bora miongoni mwa watakaojitokeza. Wakati mwingine mazingira yakiruhusu, nitaweza kutii maombi hayo”
Post a Comment