Binti wa Miaka 21 Atiwa Mbaroni kwa kuchoma moto nyumba sababu ikitajwa kuwa ni wivu wa kimapenzi
Jeshi
la polisi mkoani Singida,linamshikilia mkulima mkazi wa Mitunduruni
mjini hapa, Mariamu Juma (21), kwa tuhuma ya kuchoma nyumba moto na
kuteketea pamoja na mali zote zilizokuwemo.
Kwa mujibu wa kamanda Jeshi la Polisi mkoa wa Singida, ACP Debora Magiligimba, kitendo hicho kimechangiwa na wivu wa kimapenzi.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda Magiligimba,alisema kuwa
tukio hilo limetokea Mei 30 mwaka huu saa 11.40 jioni, huko maeneo ya
Mwenge tarafa ya Mungumaji Manispaa ya Singida.
Akifafanua,
alisema kuwa siku ya tukio mtuhumiwa alienda kwenye nyumba aliyopanga
mpenzi yake Benardo Mabula, ambayo inamilikiwa na Omari Hamisi (35)
katika maeneo ya Mwenge mjini hapa.
“Uchunguzi
wa awali wa Jeshi la Polisi umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo, ni
wivu wa kimapenzi. Mtuhumiwa Mariamu alipoingia kwenye chumba cha rafiki
yake wa kiume (Mabula),aliwasha moto kwa kiberiti kwa lengo la kuchoma
vifaa vya mpenzi wake,” alisema na kuongeza;
“Lakini
moto huo ulisambaa vyumba vyote vya nyumba hiyo na kuteketeza kila
kitu.Hadi sasa thamani ya nyumba na mali iliyoteketea, bado
haijafahamika.”
Kamanda
huyo alisema kuwa baada ya uchunguzi kukamilika, mtuhumiwa atafikishwa
mahakamani kujibu tuhuma inayomkabili. Mpenzi wa mtuhumiwa
Mariamu,amefanikiwa kutoroka na kukimbilia kusikojulikana.
“Jeshi
la Polisi mkoani hapa,linatoa wito kwa wananchi wote hasa familia zenye
migogoro ya ndoa,wafike ofisi zetu za dawati la jinsia na watoto
zilizopo kila wilaya, ustawi wa jamii na viongozi wa dini, ili waweze
kusikilizwa matatizo yao, badala ya kujichukulia sheria mkononi,”
alisema Magiligimba.
Katika
hatua nyingine, Kamanda huyo alisema vikongwe wawili wamefariki dunia
papo hapo, baada ya kuangukiwa na ukuta wa nyumba iliyojengwa kwa
tofali za tope na kuezekwa kwa bati.
Magiligimba
alisema vikongwe hao na watu wengine, walikuwa kwenye nyumba hiyo,
kushiriki mazishi ya Mwajuma Mwendo aliyefariki Mei, 28 na kuzikwa kesho
yake.
Aliwataja
vikongwe hao kuwa ni Nzitu Mkumbo (80) mkulima kwa kijiji cha Mwangeza
ambaye alivunjika miguu yote na mkono wa kushoto.Mwingine ni Kimwana
Kingu (90) mkulima wa kijiji cha Mazangila, ambaye alivunjika mguu wa
kulia na kujeruhiwa vibaya mguu wa kushoto. Vijiji hivyo vipo wilaya ya
Mkalama.
Aliwataja
waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni Fatma Alli (70), Zena Ntoga (40),
Kimwana Mohammed (70), Gyoli Kingu (45), Habiba Hussein (40) na Sophia
Mashimba (50).
Alisema
chanzo cha tukio hilo ni uchakavu wa nyumba hiyo iliyoanguka baada
kupigwa na upepo mkali na kusababisha ukuta wa ndani uliotenganisha
chumba na sebule, kuanguka.
“Jeshi
la polisi mkoa wa Singida,linatoa wito kwa wananchi wote wawe na
utaratibu wa kukarabati nyumba zao mara kwa mara.Pia tunawashauri
wapande miti kwa wingi kuzunguka maeneo ya makazi yao,” alisema kamanda
Magiligimba.
Post a Comment