Header Ads

Ni mechi ya kudhihirisha au kupotea kwa Azam FC


Na Zaka Zakazi
Msimu mpya wa Ligi Kuu 2017/18 umeshaanza na leo unaingia katika raundi yake ya pili. Kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2012/13, Azam FC imeonodolewa kwenye orodha ya timu zinazopewa nafasi ya ubingwa.
Wachambuzi, mashabiki na hata baadhi ya vyombo vya habari wanaiangalia Azam FC kama timu itakayopigania kukwepa kushuka daraja zaidi kuliko kupigania ubingwa. Sababu kubwa ni simulizi zinazoendelea mtaani kuhusu mabadiliko ya sera za uendeshaji wa timu kutoka kumwaga mamilioni mpaka kubana matumizi kunakochukuliwa kama sababu ya kuondoka na wachezaji wake muhimu.
Baada ya kunusurika kushuka daraja katika msimu wake wa kwanza, 2008/09, Azam FC ilijipambanua kama timu ya tajiri mkubwa kwa kuvunja benki na kukusanya wachezaji nyota.
Mrisho Ngassa alivunja rekodi ya uhamisho kutoka Yanga, Kali Ongala akarudishwa nyumbani kutoka Sweden na nahodha wa Rwanda, Patrick Mafisango akashushwa Chamazini, bila kumsahau Peter Ssenyonjo kutoka Uganda.
Usajili huu ukaibadilisha Azam FC na msimu wake wa pili, 2009/10 na wa tatu, 2010/11, ikamaliza katika nafasi ya tatu. Baada ya hapo timu hii ikaanza kupigania ubingwa na misimu miwili mfululizo ya 2011/12 na 2012/13 ilimaliza katika nafasi ya pili. Hatimaye 2013/14 ikachukua ubingwa!
Azam FC ikaendelea kuwa tishio licha ya kukosa ubingwa mpaka msimu huu ndipo mitazamo ya watu imebadilika na kuiondoa katika orodha ya wababe.
Sababu kubwa inawazowaaminisha watu kwamba timu hii itafulia msimu huu ni kuondoka kwa wachezaji 5 muhimu; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Gadiel Michael, Erasto Nyoni na John Bocco.
MTAZAMO WANGU
-Niliwahi kuongea na Hans van der Pluijm aliporudi Yanga kwa mara ya pili Disemba 2014 baada ya kuwa aliondoka Juni mwaka huo. Nilimuuliza kuhusu Yanga aliyoikuta kwa kulinganisha na ile aliyoicha alipoondoka. Akasema ameumia kutowakuta Kavumbagu, Domayo na Kiiza. Lakini timu ni kama familia, akifariki mwanafamilia mmoja, mnahuzunika halafu mnaendelea na maisha. Na yeye atafanya hivyo hivyo.
Ni kweli, Azam FC imeondokewa na wachezaji muhimu kikosini na kuondoka kwao lazima kutaacha mapengo. Lakini kama alivyosema Hans, maisha ni lazima yaendelee na katika kufanya hivyo, Azam FC imesharekebisha baadhi ya mapungufu kwa kuziba mapengo huku mapungufu na mapengo mengine yakijikebisha yenyewe
i. Aishi Manula
Huyu ni kipa bora misimu miwili iliyopita na amekuwa namba moja wa Azam FC tangu Machi 19, 2014 kwenye mchezo dhidi ya Yanga uliomalizika kwa sare ya 1 -1 huku yeye akiokoa penati ya Hamis Kiiza. Aishi pia ni kipa namba moja wa Taifa Stars. Msimu uliopita ambao ulikuwa wa hovyo zaidi kwa Azam FC tangu ule wa kwanza wa 2008/09 waliomaliza katika nafasi ya 8, Aishi alicheza mechi 29 huku mechi 14 akitoka bila kuruhusu bao. Hizi ni takwimu za kiwango cha juu zinazoweza kukuonesha huyu ni kipa wa daraja lipi.
Pengo lake lilivyozibwa
Kuondoka kwa Aishi kumewalazimu Azam FC kumsajili kipa namba moja wa timu ya taifa ya Ghana ya michuano ya Chan, Razak Abalora, kutoka klabu ya WAFA SC. WAFA SC ni timu inayomilikiwa na akademi ya WAFA(West Africa Football Academy) iliyopo chini ya klabu ya Feyenoord ya Uholanzi. Hii ni akademi kubwa kuliko zote Afrika Magharibi.
Mpaka anasajiliwa Azam FC, Razak(20) alikuwa ameshacheza mechi 22 za ligi kuu huku mechi 12 akitoka bila kuruhusu bao.
Kuwa kipa namba moja wa timu ya taifa ya Ghana (japo ni ya CHAN) siyo kitu cha kubeza hivyo usajili wa kipa huyu unatoa uhakikisho kwamba nafasi ya Aishi imezibwa vilivyo.
ii. Shomary Kapombe
-Ni ngumu kumpata mtu kama Kapombe kutokana na uzoefu na uwezo wake. Unapokuwa na Kapombe uwanjani unakuwa na zaidi ya beki wa kulia; ni kiongozi, ni kiungo na ni mshambuliaji. Mabao yake 8 aliyofunga msimu wa 2015/16, ni ushahidi tosha kuonesha alivyo hatari sehemu zote za uwanja.
Pengo lake lilivyozibwa
Katika kuziba mapengo ya wachezaji wa aina hii, mara nyingi kinachohitajika siyo mchezaji mbadala wa sifa za aliyeondoka bali majukumu wanayopewa uwanjani. Kocha anaweza akabadilisha mbinu ya uchezaji itakayomfanya atakayechukua nafasi ya aliyeondoka kuyamudu majukumu bila shida kubwa. Moja ya mbinu hapa huwa kutafuta winga mwenye asili ya ulinzi ili awe anashuka kumsaidia huyo mbadala.
Kwa Azam FC, upande wa Kapombe yupo Danny Amoah. Huyu jamaa alikuwa beki wa timu ya Medeama ya Ghana ambayo ilikuwa kundi moja na Yanga robo fainali ya kombe la shirikisho la Afrika. Yanga walifungwa 3-1 na Medeama yeye akifunga bao la kwanza. Itakumbukwa kwamba Yanga ile ilikuwa ya kihistoria. Iliweka rekodi hapa nchini kwa kutwaa ubingwa ikiwa na pointi nyingi zaidi kuwahi kutokea.
Katika kundi lao, Medeama walimaliza wa tatu kwa pointi zao 8, wakizidiwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa na waliomaliza katika nafasi ya pili, Mo Bejaia ya Algeria ambayo ilifika fainali na kufungwa na TP Mazembe ambayo pia ilikuwa kundi hilo hilo. Medeama ilikuwa timu pekee kuifunga TP Mazembe kwenye kundi lao. Beki anayetegemewa na timu ya aina hii siyo wa kuchukuliwa poa.
Lakini pia upande huu yupo Swalehe Abdallah. Kijana huyu aliyetokea Kahama na kujiunga na akademi ya Azam FC mwaka 2012 sambamba na Aishi Manula, Ismail Gambo na Braison Rafael, alianzia nafasi za mbele kabla ya kubadilishwa kuwa beki na kocha wa vijana wakati huo, Vivek Nagul. Alianza kama beki wa kati na baadaye akawa beki wa kulia.
Bahati mbaya kwake ilikuwa uwepo wa watu watatu kwenye eneo lake, Erasto Nyoni, Malika Ndeule na Mgaya Abdul(mdogo wa Juma Abdul wa Yanga).
Kuna wakati alikaribia kwenda Yanga lakini sijui nini kilitokea, akaenda Stand Utd halafu Majimaji. Msimu huu, baada ya Azam FC kushindwa kumpata Salum Kimenya wa TZ Prisons, wakaamua kumrudisha kijana wao huyu Chamazini.
Uzoefu wake wa kucheza mbele ambako ndiko alikoanzia, na beki wa kati aliporudi nyuma, vinaweza kumsaidia kuyamudu majukumu mapya ndani ya kikosi cha Azam FC. Kumbuka bao alilofunga dhidi ya Onduparaka FC kule Uganda kwenye pre season, ni la kiwango cha mshambuliaji mzoefu, siyo beki…ni kama alivyokuwa akifanya Kapombe.
3. Gadiel Michael
Ni mmoja wa wachezaji wa akademi aliyetoa mchango mkubwa kwenye msimu wa ‘unbetean run’ ambao Azam FC walichukua ubingwa bila kupoteza mchezo hata mmoja na kuingia katika vikosi vya ‘Invicibles’. Gadiel pia ni beki tegemeo kwa sasa katika timu ya taifa, Taifa Stars.
Pengo lake lilivyozibwa
Katika wachezaji muhimu wa Azam FC waliondoka msimu huu, Gadiel ni mchezaji aliyekuwa na umuhimu mdogo zaidi. Nafasi yake haihitaji nguvu nyingi kuiziba kwa sababu hakuwa mchezaji wa kuweza kutegemewa msimu mzima. Gadiel ni mchezaji asiye na ‘consinstence’ yaani muendelezo wa kiwango. Mara zote amekuwa na homa za vipindi.
Kuna wakati huwa anakuwa kwenye ‘fomu’ ya hali ya juu halafu anashuka mpaka kiwango cha chini kabisa. Katika kipindi chake chote cha ‘maji kupwa maji kujaa’, nafasi yake ilikuwa chini ya ‘kiraka’ Erasto Nyoni. Hii ikaendelea mpaka akasajiliwa Bruce Kangwa kutoka Zimbabwe. Kangwa, mchezaji aliyekuwa kwenye kikosi cha Zimbabwe kilichoshiriki AFCON 2017, ni wa daraja la juu zaidi kuliko Gadiel. Ila kwa kuwa tayari Gadiel alikuwepo wakati ule, na Kangwa alikuwa na uwezo wa kucheza kama winga tangu akiwa kwao, akaanza kwa kutumika mbele, lakini kwa sasa atarudi chini na kumfanya Gadiel asaulike kabisa. Nafasi atakayoiacha kule mbele kushoto itazibwa na Enoch Atta Agyei ambaye msimu huu ataitumikia Azam FC baada ya kubanwa na kanuni hapo kabla licha ya kusaijiliwa tangu 2016.
4. Erasto Nyoni
Kwa sasa hapa nchini hakuna mchezaji kiraka kama Erasto Nyoni. Huyu jamaa anacheza karibu nafasi zote kasoro kudaka tu. Kwa kifupi, Erasto ni ‘most complete technical player’ hapa nchini. Anaweza akaingia kwa ajili ya kuifanya kazi moja tu, kumpoteza ‘mtu hatari’ uwanjani.
Kocha wa sasa wa Man U, Jose Mourinho, alikuwa na msemo wake wakati akiwa Chelsea katika awamu yake ya kwanza, ‘make it 10 against 10’, yaani kuifanya mechi kuwa ya wachezaji 10 kwa 10. Kama wapinzani walikuwa na mchezaji hatari, alikuwa anamtuma Geremi Njitap kwenda kumpoteza na kupotea naye. Hapo anakuwa ameifanya mechi iwe ya wachezaji 10 kwa 10 badala ya 11 kwa 11. Geremi akiingia, anampoteza mtu na yeye anapotea…waliobaki ndiyo wanaocheza, na Erasto pia kazi hii anaiweza kwa uzuri wa kutosha.
Pengo lake linavyozibwa.
Licha ya ubora wote huo wa Erasto, ni vigumu kumuona kama mchezaji muhimu kwenye timu kwa sababu hana namba maalumu atakayoacha pengo. Yeye amekuwa akitumika kuziba mapengo ya wengine kwa hiyo wenyewe wakiwepo, yeye haonekani muhimu. Hii ni sehemu moja na kubwa sana ya mchezaji kama huyu kutoacha pengo anapoondoka.
5. John Bocco
Hakuna ubishi kwamba huyu jamaa alikuwa muhimu zaidi kwa Azam FC kuliko wengine wote walioondoka. Siyo kwa sababu ya historia yake bali mchango aliokuwa akiendelea kuutoa ndani na nje ya uwanja.
Wachezaji wenzake walikuwa wanamuita Mr. Azam FC na uwepo wake ulikuwa muhimu kila wakati. Mwaka 2016, Azam FC walitoka sare ya 2-2 na JKT Ruvu. Azam waliongoza 2-0 kipindi cha kwanza lakini zikarudi zote kipindi cha pili. Baada ya mchezo huu, John Bocco alibaki peke yake kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, akilia kwa uchungu. Matokeo yalimuumiza sana. Matukio kama haya kwa Bocco ni mengi mno kwa sababu aliamini Azam FC ni sehemu ya damu yake.
Lakini vitu vizuri vyote hufikia wakati vinaisha na hivyo hivyo kwa nyakati nzuri za John Bocco Azam FC zikafikia mwisho.
Pengo linavyozibwa
Tangu alipokuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu wa 2011/12, Bocco amekuwa kinara wa mabao kwa Azam FC kila msimu kasoro mmoja tu, 2012/13 ambapo pacha wake Kipre Tchetche alimzidi klabuni na kwenye ligi kwa ujumla.
Kuziba pengo la mtu kama huyu haiwezekani hata kidogo. Arsenal hawatakuja kuziba pengo la Henry, Barcelona hawatakuja kuziba pengo la Messi. Ila kwa kuwa maisha ni lazima yaendelee, Azam FC imesajili washambuliaji kadhaa wanaoweza kuleta mabao Chamazini.
i. Mbaraka Yusuph
-Mabao yake 12 msimu uliopita yanatoa ishara kwamba Azam FC wanaweza kufaidika naye katika maisha yao mapya. Zaidi ya kufunga tu, Yusuph pia ni mzuri kwenye kuumiliki na kuudhibiti mpira, anaweza kuwahadaa mabeki na anapiga kwa miguu yote. Akifunga kuanzia mabao 7 atakuwa amepunguza machungu ya kumkosa Bocco kwa kiasi fulani.
ii. Waziri Junior
-Alimaliza msimu uliopita kwa mabao 7 akiwa na timu yenye viungo wanaotoa msaada hafifu Toto Africans. Endapo atatulia na kuweka akili zake kwenye kuzipasia nyavu za wapinzani, huku akipata msaada kwa viungo wenye uwezo mkubwa kuliko aliocheza nao msimu ulipoita anaweza akasaidia kupunguza mzigo wa majonzi ya kuondoka kwa Bocco.
iii. Yahaya Zayd
Ni wonder kid aliyeibuka kutoka akademi, kule kule walikotoka wakina Aishi Manula na Gadiel Michael.
Msimu uliopita alipelekwa kwa mkopo Ashanti United alikofunga mabao 9 ligi daraja la kwanza.
Kwenye mechi za kujiandaa na msimu mpya, amefunga takribani mabao 5, kuanzia Iringa dhidi ya Lipuli mpaka Uganda. Kama ataifungia Azam FC mabao kuanzia 5 kwenye ligi kuu, utakuwa msaada mkubwa sana kwao.
Washambuliaji hawa wakisaidiana na waliokuwepo hapo kabla, wanaweza kuisaidia pakubwa sana klabu hii
i. Shaban Idd Chilunda
alifunga mabao 7 msimu uliopita na kuwa mfungaji bora namba mbili wa klabu, mabao 2 nyuma ya John Bocco. Alianza kupata nafasi ya uhakika mzunguko wa pili wa ligi baada ya kuumia John Bocco kwenye mchezo dhidi ya Simba SC Januari 28 ambapo Bocco mwenyewe alifunga bao la ushindi. Msimu huu anaweza kufanya kitu kikubwa zaidi kutokana na angalau kuizoea ligi kidogo.
ii. Yahaya Mohamed
Huyu ni mfungaji bora wa ligi ya Ghana msimu wa 2016. Alimaliza akiwa na mabao 16. Bahati mbaya kwake ni kwamba mambo hayakumuendea vizuri Tanzania katika msimu wake wa kwanza. Matokeo yake hata yeye mwenyewe akaanza kutilia shaka uwezo wake, hapo ndipo alipopotea.
Msimu huu anaonekana kuanza vizuri, mabao yake matatu aliyoyafunga Uganda kwenye pre season na moja la ufunguzi wa msimu dhidi ya Ndanda FC, yanaweza kumjenga kisaikolojia kwa kiwango kikubwa na kumrudishia kujiamini kwake kulikopotea msimu uliopita.
Kikubwa ambacho watu wengi hawakiangalii aidha kwa makusudi au bahati mbaya kwa Azam FC ni kwamba timu hii ilikuwa na kikosi kipana chenye wachezaji wawili mpaka watatu kwenye namba moja, tena wa kiwango cha juu sana. Tatizo ni kwamba huwezi kupanga wachezaji 13 uwanjani hivyo wengine wakawa wanakosa nafasi kwa sababu walimu huwa na tabia ya kukariri wachezaji.
Kila jambo zuri huwa na upande wa pili ambao huwa siyo mzuri, hali kadhalika kwa jambo baya, nalo huwa lina upande wake wa pili ambao huwa ni mzuri. Kuondoka kwa walioondoka ndani ya Azam FC ni jambo baya lakini lina upande wake wa pili ambao ni mzuri.
i. Kunapunguza presha.
Azam FC imekuwa ikihesabiwa kama timu ya ubingwa kwa misimu mitano sasa. Hii iliwaongezea presha wao wenyewe kutaka kuthibitisha heshima waliokuwa wakipewa. Ikitokea wakakosa matokeo, wanaharibikiwa vichwa. Pia ilisababisha mechi zao zote ziwe ngumu sana kwa sababu wapinzani wao walijiandaa kucheza na timu yenye hadhi ya bingwa.
Kwa sasa presha hii haipo tena kwa sababu ule mzigo wameutua. Timu zinaweza kuingia uwanjani dhidi ya Azam FC zikijiamini zinakwenda kucheza na kibonde mwenzao. Hii ndiyo iliyoisaidia Leicester City kuwa bingwa 2016.
ii. Nafasi kwa wengine
Kuondoka kwa waliondoka kunakunatoa mwanya kwa waliokuwa wakikosa nafasi, kutoa mchango wao. Pia maeneo muhimu ya timu, kama kiungo na safu ya ulinzi, kwa asilimia kubwa imebaki na watu wale wale.
i. Yakub Mohamed
ii. Aggrey Moris
iii. Himid Mao
iv. Sure Boy
v. Kingue Mpondo
Hawa ni mihimili ya Azam FC na bado wapo kwenye timu. Lakini hayo yote yataanza na mechi ya leo.
Ni mechi ya kudhihirisha au kupotea kwa Azam FC.

No comments