Header Ads

BUNDESLIGA, KINAWAKA TENA LEO


KAMA kawaida Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga, inaendelea tena wikiendi hii kwa timu zote 18 kuingia uwanjani kutafuta pointi tatu muhimu. Bundesliga ni kati ya ligi bora zaidi duniani, ikiwa inatoa wachezaji wengi sana mahiri, lakini kwa miaka kadhaa sasa timu zake zimekuwa zikifanya vizuri sana kwenye michuano mikubwa Ulaya ambayo ni Ligi ya Mabingwa Ulaya, jambo ambalo linaonyesha kuwa ni kati ya zile bora zaidi.

Wikiendi hii kwa mashabiki wa soka wa Tanzania ambao wanatumia King’amuzi cha Startimes, ambacho kimekuwa kikirusha mechi hizo moja kwa moja, yaani Live, au wengine wanasema Mubashara, watakuwa sebuleni kwao kutazama mechi kadhaa kubwa ambazo zitaanza kuonyesha picha halisi ni timu gani inaweza kufanya vizuri mwishoni mwa msimu.

Ukiachana na mchezo wa jana usiku kati ya Hamburger dhidi ya wabishi RB Leipzig, kipute cha leo ndiyo kinaonekana kuwa hatari zaidi. Pamoja na mechi
zote kuwa kali, lakini mashabiki wanasubiri kwa hamu mechi kati ya Hoff enheim ambao watawakaribisha Bayern München kwenye Uwanja wa Wirsol RheinNeckar-Arena.

Mechi hii inasubiriwa kwa hamu kutokana na ukweli kwamba Hoff enheim wanatakiwa kuhakikisha wanashinda mchezo huu baada ya kushinda mmoja na kutoka sare mmoja kwenye miwili iliyopita ya ligi hiyo.

Lakini Bayern wenyewe watataka kuwaonyesha mashabiki wa Startimes na wengine wote duniani kuwa wapo imara kwa kuwa wenyewe wameshashinda kwa asilimia 100 kwenye michezo yao miwili iliyopita. Pia watataka kuongeza kasi zaidi ili kuhakikisha wanashinda kwa mabao mengi na kuwaondoa Ujerumani Borussia Dortmund kileleni huku staa wao Robert Lewandowski akiendelea kutikisa nyavu kwani kwa sasa mechi mbili tu tayari yupo kileleni akiwa na mabao matatu.

Mechi hii itapigwa saa moja jioni kuwapa nafasi mashabiki wengi sana kutazama wakiwa nyumbani. Lakini mapema kutakuwa na kipute cha heshima, wanaume Freiburg wenyewe watakuwa nyumbani wakiwakaribisha Dortmund kwenye uwanja wao wa Schwarzwald. Hii ni mechi nyingine ambayo inasubiriwa kwa hamu kutokana na uwezo wa Dortmund ambayo imekuwa ikitoa upinzani mkubwa kwenye Bundesliga kwa miaka kadhaa iliyopita.

Hii kama zilivyo mechi nyingine nyingi itakuwa saa kumi na nusu jioni, Dortmund watakwenda kwenye mchezo huu wakiwa na pointi sita na hivyo watakuwa na tahadhari kubwa sana. Freiburg wenyewe walikuwa hawapewi nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye Bundesliga msimu huu, lakini kweli matokeo yao yamekuwa hivyohivyo. Katika michezo miwili ambayo walicheza kuanzia msimu huu umeanza wamefanikiwa kukusanya pointi moja tu kati ya sita wakiwa wanashika nafasi ya 15 kwenye ligi hiyo yenye timu 18.

Kama watapoteza mchezo huu basi watakuwa wamejiweka kwenye mazingira magumu sana, Dortmund bado watakuwa wakimtegemea staa wao Pierre Aubameyang ambaye kwenye michezo miwili tayari ameshafunga mabao mawili, wastani wa bao moja kwenye kila mchezo. B o r u s s i a M’gladbach, ambao wanashika nafasi ya tano kwenye ligi hiyo wanatarajiwa kuwavaa Eintracht Frankfurt kwenye Uwanja wa Borrusia Park.

Frankfurt wanaingia kwenye mechi hii wakimtegemea staa wao Luka Jović na kocha wao ameshasema kuwa ili kujua kama wanaweza kupambana kwenye msimu huu wa ligi basi wanatakiwa kushinda mchezo huu.

Mechi nyingine za leo ni Augsburg dhidi ya Köln huku Mainz 05 wakiwakaribisha Bayer Leverkusen. Mechi za kesho Jumapili, Hertha watakuwa wenyeji wa Werder Bremen kwenye Uwanja wa Berlin, huku Schalke wakiwaita Stuttgart kwenye Uwanja wa Veltins-Arena.

CREDIT: GAZETI LA CHAMPION

No comments